Timu ya taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars, itafungua kampeni za kuwania kombe la CHAN kwa mara ya kwanza itakaposhuka uwanjani Kasarani Jumapili kuanzia saa tisa dhidi ya mabingwa mara mbili, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo.
Kenya inashiriki mara ya kwanza huku DRC, wakishiriki kwa mara ya saba, wakikosa fainali moja tu tangu kuasisiwa kwa kipute hicho mwaka 2009.
Harambee Stars na the Leopards watakutana kwa mara ya nane Jumapili, Kenya wakishinda mechi mbili, DRC wakaibuka washindi mara nne, huku mchuano mmoja ukimalizikia sare.
DRC iliwashinda Kenya bao moja kwa bila katika mechi nne walizokutana mwaka 2011, mbili za kirafiki na mbili za kuwania kombe la Nile Basin.
Kenya iliwashinda DRC bao moja kwa bila katika mchuano wa kirafiki mwaka 2016 na kufuatiliza kwa ushindi mwingine wa 2-1 dhidi ya Chui katika mechi ya kujipima nguvu mwaka 2017.
Mara ya mwisho kwa timu hizo mbili kukutana ilikuwa mwaka 2019, katika mechi ya kirafiki iliyomalizia sare ya bao 1-1.
Kenya walifuzu kwa CHAN kama moja ya waandalizi watatu.
Mataifa mengine kundini A pamoja na Kenya na DRC ni Angola, Morocco, na Zambia.