Hamisa Mobeto achumbiwa na kutolewa mahari

Nikka ya wawili hao inaandaliwa leo jijini Dar es Salaam nchini Tanzania.

Marion Bosire
2 Min Read

Jana Jumamosi Februari 15, 2025 ilikuwa siku kubwa kwa msanii na mfanyabiashara wa Tanzania Hamisa Mobeto, pale alipovishwa pete ya uchumba na kutolewa mahari na mpenzi wake Stephane Aziz Ki.

Aziz ambaye ni mchezaji soka wa klabu ya Yanga nchini Tanzania alikua ameandamana na watu wa familia yake na wachezaji wenza katika Yanga FC pamoja na viongozi wa timu.

Mzaliwa huyo wa Ivory Coast anayechezea timu ya taifa ya Burkina Faso, na ambaye pia ni mchezaji wa kulipwa wa Yanga amekuwa akionyesha ukaribu wa pekee na Hamisa lakini waliuita urafiki tu.

Pete aliyomvisha Hamisa inaripotiwa kugharimu pesa nyingi sana na ng’ombe waliojaa malori matatu yalikuwa sehemu ya mahari ya Hamisa.

Hafla hiyo ilijaa furaha na kwa wakati mmoja Hamisa alizidiwa na hisia akatiririkwa na machozi pale ambapo Aziz alipowakumbatia wanawe.

Hamisa ana watoto wawili wa kwanza wa kike kwa jina Fantasy ambaye babake ni Majizzo na wa pili ni Dylan ambaye babake ni mwanamuziki Diamond Platnumz.

Aziz naye ana mtoto mmoja na binti fulani wa Tanzania.

Wanamitandao nchini Tanzania wamefurahikia ndoa ya Hamisa wakisema alidhalilishwa sana na wapenzi wake wa awali na sasa ameheshimishwa na Aziz Ki.

Leo Jumapili Februari 16, 2025, Aziz na Hamisa wanatarajiwa kufunga ndoa chini ya taratibu za dini ya kiisilamu inayofahamika kama Nikka.

Ndoa hiyo itasherehekewa rasmi Februari 19, 2025.

Kulingana na Juma Lokole, Aziz anaharakisha mipango ya ndoa na Hamisa kwani anahamia nchi nyingine kwa ajili ya soka ya kulipwa.

Share This Article