Mlinzi wa klabu ya PSG na Morocco Achram Hakimi, alitawazwa mchezaji bora wa soka mwaka huu kwenye tuzo za kufana zilizoandaliwa Jumatano usiku jijini Rabat, Morocco.
Rai wa Morocco walitawala tuzo hizo ambazo ziliandaliwa katika taifa hilo la Kaskazini mwa Afrika kwa mara ya tatu mtawalia.
Hakimi alishinda tuzo hiyo kwa mara ya kwanza kutokana na mchango wake mkubwa kwa PSG kutwaa taji ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu Ufaransa, Kombe la Ufaransa, na UEFA Super Cup, na kucheza hadi fainali ya Kombe la Dunia kwa vilabu.
Beki huyo wa kulia mwenye umri wa miaka 27 aliwashinda washambulizi Mo Salah wa Misri na Liverpool na Victor Osimhen wa Nigeria na klabu ya Galatasaray.
Ghizlane Chebbak, wa klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia pia kutoka Morocco, alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka kwa wanawake huku Chiamaka Nnadozie kutoka Nigeria akihifadhi tuzo ya kipa bora kwa mwaka wa tatu kwa mpigo.
Yassine Bonou wa Morocco na klabu ya Al Hilal alinyakua tuzo ya kipa bora wa mwaka, naye Fiston Mayele wa DR Congo akiibuka mchezaji bora kwa wale wanaopiga soka barani Afrika.