Hackman, mkewe wapatikana wamefariki nyumbani

Walipatikana wameaga nyumbani kwao alasiri ya Jumatano Februari 26, 2025 kulingana na saa za Marekani.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwigizaji wa Marekani Gene Hackman na mke wake Betsy Arakawa wamepatikana wakiwa wamefariki nyumbani kwao katika jimbo la New Mexico nchini Marekani.

Afisi ya mwanasheria mkuu wa Santa Fe ilithibitisha taarifa hizo ikielezea kwamba wawili hao walipatikana wakiwa wameaga nyumbani kwao alasiri ya Jumatano Februari 26, 2025 kulingana na saa za Marekani.

Polisi wamesema kwa sasa wanachunguza kilichosababisha kifo cha mshindi huyo wa tuzo ya Oscar na mke wake lakini hawaamini kwamba kilikuwa kitendo cha uhalifu.

Nyota huyo wa tasnia ya uigizaji na burudani nchini Marekani, Hollywood, amefariki akiwa na umri wa miaka 95. Aliwahi kupokea tuzo mbili za Oscar na mbili za Bafta katika uigizaji wake wa miongo kadhaa.

Tuzo ya kwanza ya Oscar katika kitengo cha mwigizaji bora aliipokea mwaka 1972 kutokana na igizo lake kama Detective Jimmy “Popeye” Doyle katika filamu iitwayo ‘The French Connection’ ya mwaka 1971.

Tuzo nyingine ya Oscar ya mwigizaji bora msaidizi alipokea mwaka 1992 alipoigiza kwenye filamu ‘Western Unforgiven’ ya mwaka huo wa 1992 iliyoelekezwa na Clint Eastwood.

Kazi hizo hizo ndizo zilimshindia tuzo katika vitengo sawia katika tuzo za filamu za Uingereza Bafta.

Share This Article