Guyo ahimiza ODPP itoe ushahidi wa kumhusisha na utekaji nyara

Marion Bosire
1 Min Read
Abdi Guyo - Gavana wa Mandera

Gavana wa kaunti ya Isiolo Abdi Ibrahim Guyo amehimiza afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini ODPP, itoe ushahidi wa kumhusisha na madai ya utekaji nyara na wizi wa kimabavu.

Haya yanafuatia hatua ya ODPP ya kuagiza akamatwe na kufunguliwa mashtaka kuhusiana na utekaji nyara na uporaji uliokumba mpinzani wa Guyo kwa jina Abdirahaman Mohamed.

Kisa hicho kinadaiwa kutokea katika hoteli ya Outbark iliyoko Maanzoni katika kaunti ya Machakos ambako wawakilishi wadi wa kaunti ya Isiolo walikuwa na mkutano.

Guyo anadai kwamba ODPP haina ushahidi inaodai wa kumhusisha na kisa hicho akisema siku ya tukio yeye alikuwa Nakuru na alipotoka huko alienda nyumbani kwake.

Lakini katika taarifa ya kuagiza akamatwe, mkurugenzi mkuu wa ODPP Renson Ingonga alidokeza kwamba kuna ushahidi wa video iliyonaswa na kamera za ulinzi za hoteli ya Outbark.

ODPP ilielezea kwamba Guyo alionekana hotelini humo na alisikika akitoa maagizo ya kutwaliwa kwa Abdirahaman na kupelekwa katika eneo la Ruai.

Inadaiwa pia kwamba katika purukushani hiyo, mwakilishi wadi huyo alipoteza vitu vya thamani zikiwemo pesa taslimu shilingi elfu 70.

Tayari Guyo na washukiwa wenza wamepata maagizo kutoka kwa mahakama kuu ya Kiambu ya kuzuia kukamatwa kwao kuhusiana na kisa hicho.

Share This Article