Gurudumu la maisha Chongqing – Uhalisia wa tambi kali za Chongqing

Katika kila bakuli la tambi kali, kuna ladha ya urithi wa kitamaduni na falsafa ya maisha ya watu wa Chongqing.

Eric Biegon
3 Min Read
Highlights
  • Maelezo ya Mhariri Makala haya yameandaliwa kwa ushirikiano na taasisi ya masomo ya kigeni ya Chongqing kama sehemu ya mfululizo wa ripoti zinazochunguza utajiri wa urithi wa kitamaduni usioshikika wa jiji hilo.

Watu wa Chongqing hupenda kusema kwamba mtu anaweza kuelewa zaidi kuhusu ulimwengu baada ya glasi ya pombe kali, na vivyo hivyo, mtu anaweza kufahamu kwa kina maisha baada ya kula bakuli la tambi kali.

Mitaa na kona za manispaa ya Chongqing zimejaa vibanda vya kuuza tambi au migahawa midogo, ambapo mtu anaweza kuhisi haiba ya kipekee ya jiji hili na kuelewa mtazamo wa wakazi wake kuhusu maisha.

Tambi kali za Chongqing hujulikana kama “Gang Zi noodles”, jina linalotokana na njia ya kutengeneza unga kwa kutumia mianzi au kijiti cha mbao. Utengenezaji wake unachanganya mbinu kutoka sehemu mbalimbali za China kama vile kukanda, kukata na kuvuta.

Kwa mujibu wa Liu Yidian, mrithi wa tambi kali za Chongqing, kuna zaidi ya hatua 20 kuanzia kusaga ngano hadi kutayarisha chakula mezani.

Hatua ya kwanza ni kutengeneza tambi kwa kuchanganya unga na maji, kukanda, kusambaza, kisha kukata. Kazi hii ya kukanda hufanywa kwa nguvu ya wastani mara kadhaa ili kuhakikisha tambi zinakuwa na mvuto wa kipekee (al dente). Hatua inayofuata ni utayarishaji wa kichemsha ladha (seasoning) – ambayo ndiyo moyo wa ladha ya tambi hizo. Kawaida, hutumia gramu 10–15 za mchuzi wa soya, gramu 2 za unga wa kuku (chicken powder), gramu 2 za viungio vya ladha (gourmet powder), gramu 30 za mafuta ya pilipili ya Chongqing, gramu 2 za unga wa pilipili ya Sichuan, gramu 8 za maji ya tangawizi na kitunguu saumu, gramu 10 za mafuta ya nguruwe au mboga, pamoja na vitunguu maji, mboga ya haradali iliyochachushwa, na mbegu za ufuta.

Kisha hatua inayofuata ni kupika supu. Mifupa ya nguruwe na kuku waliokomaa huchemshwa kwa saa mbili, pamoja na maharagwe mabichi ya soya, mwani au uyoga mbichi. Baada ya hapo, huchemshwa kwa saa nyingine moja hadi supu ibadilike kuwa nyeupe kama maziwa. Tambi hupikwa kwa dakika mbili au tatu, kisha kuwekewa supu na viungo tayari kwa kuliwa.

Liu anasisitiza kuwa uzoefu na ustadi wa mikono ni muhimu sana katika kutengeneza bakuli la tambi kali linalokidhi ladha ya kila mteja.

Uhai na msisimko wa Chongqing hauonekani tu kwenye vibanda vya tambi barabarani, bali pia mioyoni mwa warithi wa urithi huu wa kitamaduni usiogusika.

Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na ichongqing.info

Share This Article