Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Kenya, Gor Mahia, watamenyana na klabu ya Nairobi City Stars, katika mechi ya raundi ya 30 ya Ligi Kuu leo kuanzia saa kumi alasiri katika uwanja wa Dandora.
Gor, walio katika nafasi ya tatu kwa alama pointi sita nyuma ya viongozi Police FC, watalenga ushindi ili kupunguza pengo dhidi ya Police waliosakata mechi mbili zaidi ya The Green Army.
Juhudi za Maafande kutwaa ubingwa zilitiwa na dosari baada ya kaumbulia kipigo cha 2-1 ugenini dhidi ya Kakamega Homeboyz jana.
Katika mchuano wa awali ugani Dandora leo Kenya Commercial Bank, watakumbana na Kariobangi Sharks, kuanzia saa saba adhuhuri.
Police FC, baada ya mechi 31 wakisalia na mechi tatu, wangali kileleni kwa pointi 58,wakifuatwa na Tusker FC kwa alama 55, huku Gor wakiwa na alama 53 moja zaidi ya Shabana iliyo ya nne.