Gloria Bugie asema analenga tuzo ya Grammy

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Gloria Bugie anajivumia ufanisi ambao ameafikia katika sekta ya muziki akisema lengo lake ni kushinda tuzo ya Grammy.

Alikuwa akizungumza katika mahojiano ambapo alisema angependa kuwakilisha Uganda kimataifa ndiposa anataka kushinda tuzo hiyo kama alivyoahidi.

“Ninataka kuiwakilisha Uganda nje ya mipaka yake. Ninataka kushinda tuzo ya Grammy kama nilivyoahidi, kwa hivyo ninataka watu wanikubali ulimwenguni kote kama ninavyokubaliwa nyumbani,” alisema.

Msanii pekee wa Uganda ambaye amewahi kuteuliwa kuwania tuzo ya Grammy ni Eddy Kenzo kupitia wimbo wake uitwao “Gimme Love” aliomhusisha Matt B.

Lakini Kenzo alishindwa kwenye kitengo cha tumbuizo bora la muziki wa ulimwengu na wanamuziki wa Afrika kusini Wouter Kellerman, Zakes Bantwini, and Nomcebo Zikode kwa wimbo wao “Bayethe” katika awamu ya 65 ya tuzo hizo mwaka 2023.

Mrembo huyo anaamini pia kwamba muziki wake umepokelewa vyema na mashabiki stahiki nchini Uganda ambao sasa wanajihusisha nao kwa kiwango kikubwa.

Alijigamba kwenye mahojiano hayo akisema yeye ndiye msanii wa muziki ambaye hupatiwa kazi nyingi za utumbuizaji akisema mara nyingine huwa anazidiwa na kiasi cha maonyesho anayofanya kwa wiki.

Gloria aliendelea kusifia kazi zake za sanaa akisema kwamba amekuwa akiona watu wakitokwa na machozi anapokuwa jukwaani kutumbuiza hali ambayo alisema inampa raha kwani inadhihirisha mapenzi.

Bugie aliangaziwa sana mitandaoni nchini Uganda baada ya kufanyiwa upasuaji wa kuboresha umbo lake la mwili almaarufu BBL.

Share This Article