Ghasia zilizuka Alhamisi alasiri wakati mwili wa marehemu Albert Ojwang ulipowasilishwa nyumbani kwao katika kijiji cha kokwanyo, kaunti ya Homa Bay.
Kundi la vijana waliokuwa na hasira lilisimamisha msafara uliobeba mwili wa Ojwang katika kituo cha kibiashara cha Lida umbali wa takriban kilomita moja kutoka nyumbani kwa familia ya Ojwang, na kupeleka mwili huo hadi kituo cha Mawego, ambapo Ojwang alizuiliwa baada ya kuchukuliwa kutoka nyumbani kwao.
Juhudi za babake Albert za kuwatuliza vijana hao hazikufanikiwa, huku mzozo huo ukidumu kwa takriban saa tatu.
Taharuki ilikithiri wakati kundi hilo lilipoondoa jeneza lililobeba mwili huo kutoka kwenye gari na kulibeba mabegani hadi kituo cha polisi cha Mawego ambako waliteketeza kituo hicho cha polisi, kuharibu bango na kuondoa vizuizi vya kiusalama.
Shughuli iliyopangwa ya kuutazama mwili huo kwenye shule ya msingi ya Nyawango ilifutiliwa mbali huku msafara huo badala yake ukielekea nyumbani kwa familia yake.
Akizungumza na wanahabari kwa njia ya simu kamanda wa kaunti Lawrence Koilem alishtumu ghasia hizo akithibitisha kwamba afisi ya ripoti za polisi, nyumba moja ya polisi na afisi ya afisa mkuu msimamizi wa kituo hicho cha Mawego ziliteketezwa wakati wa ghasia hizo.
Iliwabidi maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Kendu Bay kuingilia kati kurejesha utulivu.
Wanafunzi hao baadaye waliupeleka mwili huo nyumbani kwa Meshack Ojwang, babake Albert katika kijiji cha Nyawango. Albert Ojwang atazikwa kesho.