Gérard Depardieu ahukumiwa kifungo cha miezi 18

Kifungo chake kilichosimamishwa kinaambatana na faini ya dola elfu 32,350.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwigizaji wa Ufaransa Gérard Depardieu wa umri wa miaka 76 amehukumiwa kifungo kilichosimamishwa cha miezi 18, baada ya kupatikana na hatia ya dhuluma za kingono.

Hukumu dhidi yake imetolewa leo na kesi hiyo inatokana na kisa ambapo alimshika vibaya msimamizi wa mavazi wa umri wa miaka 54 na msaidizi wa miaka 34 katika eneo ambapo walikuwa wakiandaa filamu ya The Green Shutters ya mwaka 2021.

Kesi yake ilisikilizwa kwa muda wa siku nne mwezi Machi mwaka huu ambapo msimamizi huyo wa mavazi alielezea jinsi Depardieu alijisukulimia kwake akitumia miguu huku akimpapasa kifua na sehemu za siri.

Alimlaumu pia kwa kuonyesha nia ya kushiriki ngono naye huku akimtaka naye amshike sehemu za siri.

Msaidizi naye alisema alishikwa makalio na kifua na mwigizaji huyo mara tatu tofauti wakiwa kwenye maandalizi ya filamu hiyo.

Gérard Depardieu hata hivyo alikanusha mashtaka yote wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo lakini akakubali kwamba alitumia maneno machafu.

Hakuwa mahakamani leo wakati wa kutolewa kwa hukumu dhidi yake na wakili wake kwa jina Jérémie Assous amethibitisha kwamba watakata rufaa.

Kifungo chake kilichosimamishwa kinaambatana na faini ya dola elfu 32,350 huku mahakama ikiomba aorodheshwe kwenye hifadhidata ya wahalifu wa ngono.

Inaripotiwa kwamba wanawake zaidi ya 20 wamewahi kulalamika kuhusu tabia mbaya ya mwigizaji huyo akiwemo mwigizaji Charlotte Arnould mwaka 2018.

Share This Article