Gavana wa Nyamira abanduliwa madarakani

Marion Bosire
2 Min Read
Amos Nyaribo - Gavana wa Nyamira

Gavana wa kaunti ya Nyamira Amos Kimwomi Nyaribo, ameondolewa mamlakani na Bunge la Kaunti hiyo leo.

Wabunge 23 wa bunge la gatuzi hilo walipiga kura kuunga mkono mjadala wa hoja ya kumwondoa mamlakani kwa misingi ya ukiukaji mkubwa wa Katiba na mashtaka mengine.

Jaribio hili la tatu la kumng’atua Nyaribo linaongozwa na mwakilishi wa wadi ya Bonyamatutwa, Julius Matwere.

Hatua inayofuata sasa ni ya bunge la kaunti ya Nyamira kufahamisha bunge Seneti rasmi na Seneti itaamua kama itaidhinisha au kubatilisha uamuzi wa Bunge la Kaunti.

Iwapo uamuzi huo utaidhinishwa na Seneti, Naibu Gavana James Gesami atachukua uongozi wa Kaunti ya Nyamira.

Baadhi ya wawakilishi wadi wa kaunti ya Nyamira ambao wanamuunga mkono gavana waliamua kususia kikao hicho na badala yake wakawasilisha viapo vilivyoidhinishwa wakitangaza kutoshiriki mchakato huo.

Hati zao ziliandaliwa na kampuni ya mawakili ya Wesonga G.O & Co. Advocates na kuapishwa mbele ya maafisa wa kiapo, ambapo walielezea bayana uamuzi wa kutoshiriki na kutompa yeyote ruhusa ya kufanya lolote kwa niaba yao.

Baadhi ya wanaomuunga mkono gavana wanadai mchakato huo uliendeshwa kisiasa.

Gatuzi la Nyamira limekuwa likikumbwa na misukosuko ya uongozi wa kisiasa ikikumbukwa kwamba Enock Okero alibanduliwa kutoka wadhifa wa spika wa bunge la Kaunti na Thaddious Nyabaro akachukua mahala pake.

Septemba 2024, Evans Matunda ambaye ni mwakilishi wadi mteule wa Nyamira aliwasilisha notisi ya mjadala wa kumbandua madarakani Gavana Nyaribo, mwaka mmoja tu baada ya jaribio jingine.

Share This Article