Gavana wa Marsabit Mohammud Ali na Seneta wa Mandera Ali Roba wamenyoshewa kidole cha lawama kwa kuchochea mivutano ya kisiasa katika kaunti ya Isiolo.
Madai hayo yametolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa kutoka kaunti ya Isiolo, wakiongozwa na Gavana wa zamani wa kaunti hiyo Godana Doyo na Mwakilishi wa Wanawake Mumina Bonaya.
Viongozi hao wakitoa wito wa kuzimwa kwa mioto ya uhasama katika kaunti hiyo ili kufungua milango ya kutekelezwa kwa maendeleo yanatakayowanufaisha wakazi wa kaunti hiyo.
Wito wao unakuja siku chache baada ya Gavana wa Isiolo Abdi Guyo kukwepa makali ya shoka kali lililotishia kumbandua madarakani.
Hii ni baada ya Seneti kutupilia mbali hoja iliyopitishwa na Wawakilishi Wadi wa kaunti hiyo ya kutaka kumbandua Gavana Guyo madarakani.
Hiyo yenyewe ilitupiliwa mbali kwa msingi kwamba Wawakilishi Wadi hawakufuata utaratibu uliowekwa katika azima yao.
Siku chache zilizopita,Gavana Guyo alimshutumu vikali Seneta wa kaunti hiyo Fatuma Adan Dullo kufuatia matamshi aliyotoa bungeni kuhusu hali ya usalama Isiolo.
Guyo anamtuhumu Seneta Dullo kwa kugeuza visa vya uhalifu kuwa ajenda za kisiasa na kushambulia watumishi wa umma kama vile kamishna wa kaunti.
Aliwalaumu baadhi ya wanasiasa kwa kutumia matukio fulani kama vile hali ya usalama katika kaunti hiyo kama silaha ya kisiasa, jambo linaloweza kuchochea hisia kali kwa wananchi.
Kuhusu jaribio la kumwondoa mamlakani, Gavana Guyo aliwaambia waliopanga njama hiyo kuwa hakuna njia ya mkato kufikia kiti cha ugavana, na kwamba muda wa uchaguzi ni mwaka wa 2027 ambapo yeyote mwenye nia ya kuwania kiti hicho anatakiwa kuomba ridhaa ya wananchi wa Isiolo.
Taarifa hii imechangiwa na Kevin Wachira