Gavana wa kaunti ya Nyamira Amos Nyaribo amekanusha mashtaka yote aliyolimbikiziwa na bunge la kaunti ya Nyamira ambalo lilimbandua madarakani.
Kiongozi huyo alifika katika bunge la Seneti leo kwenye siku ya kwanza ya kusikilizwa kwa kesi yake na kukanusha mashtaka aliyosomewa na naibu karani wa bunge la Seneti Mohamed Ali.
Nyaribo analaumiwa kwa kuhusika na kuunga mkono mpango wa Bunge Mashinani kinyume cha sheria na kuidhinisha kinyume cha sheria mswada wa matumizi ya ziada wa Kaunti ya Nyamira wa mwaka 2024.
Anadaiwa pia kumteua kinyume cha kisheria wa Dkt. Peris Nyaboke Oroko kwa jina jingine Peris Mongare, kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Kaunti.
Gavana huyo anadaiwa kuteua kiholela wajumbe wa Bodi za Manispaa za Nyamira na Keroka, kuunda kinyume cha sheria Jopo la Uteuzi la Bodi ya Huduma za Umma ya Kaunti – CPSB na kukosa kuteua mwenyekiti, katibu na wajumbe wa CPSB.
Bunge la Kaunti pia linamlaumu Gavana Nyaribo kwa kutotoa hotuba ya hali ya Kaunti na Ripoti za Mwaka na kushindwa kutekeleza maagizo ya mahakama kuhusu uteuzi wa Clive Ogwora katika Kamati ya Utendaji ya Kaunti.
Kuhusu matumizi mabaya ya ofisi, bunge linamlaumu Gavana kwa kuajiri watumishi bila mgao wa bajeti, kuhusika na uteuzi usio wa kawaida wa maafisa wakuu wa rasilimali watu na kujinufaisha kupitia malipo yasiyo ya kawaida ya mishahara.
Wajumbe wa Bunge wanaeleza pia kuhusu mtandao wa udanganyifu katika orodha ya mishahara ambao unadaiwa kusababisha upotevu wa fedha za umma, kuhusika kwa Gavana katika uteuzi wa watu wawili katika nafasi moja kinyume cha mfumo halali wa ajira, na kuvuruga mamlaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na CPSB.
Gavana Nyaribo pia anatuhumiwa kwa kumsimamisha kazi kinyume cha sheria Katibu wa CPSB.
Suala la Gavana Nyaribo linasikilizwa na Seneti leo na kesho.