Mivutano imeibuka tena kati ya Gavana wa kaunti ya Meru Kawira Mwangaza na bunge la kaunti hiyo.
Hii ni baada ya Wawakilishi Wadi kuwasilisha hoja nyingine ya kutaka kumtimua madarakani Gavana huyo ambaye miezi michache iliyopita alitangaza kujiunga na chama cha UDA.
Hili litakuwa jaribio la tatu kwa Wawakilishi Wadi hao kutaka kumbandua Gavana Mwangaza madarakani baada ya majaribio mawili ya awali kukataliwa na bunge la Seneti.
Wakati huu, miongoni mwa masuala mengine, Wawakilishi Wadi wanamtuhumu Gavana Mwangaza kwa ubadhirifu wa rasilimali za kaunti hiyo na kuajiri wafanyakazi kupitiliza katika ofisi yake.
Uwasilishaji wa hoja hiyo unakuja wakati ambapo watu tisa kutoka kaunti hiyo wamemwandikia barua Rais William Ruto wakimtaka kuivunja serikali ya kaunti ya Meru kwa madai kuwa utoaji huduma katika kaunti hiyo umetatizwa.