Gavana Mutai apinga uhalali wa kura za kumwondoa madarakani

Shahidi wake wa kwanza katika kesi yake katika bunge la Seneti alisema idadi inayohitajika kisheria ya thuluti mbili za wawakilishi wadi haikuafikiwa katika upigaji kura huo.

Marion Bosire
2 Min Read

Gavana wa kaunti ya Kericho amepinga uhalali wa kura zilizopigwa katika bunge la kaunti hiyo kwa hoja ya kumbandua madarakani.

Kulingana na shahidi wake wa kwanza katika kesi yake inayoendelea katika bunge la Seneti, idadi inayohitajika kisheria ya thuluti mbili za wawakilishi wadi haikuafikiwa katika upigaji kura huo.

Shahidi huyo kwa jina Martin Cheruiyot Kiplagat ambaye ni mwakilishi wadi aliambia bunge la Seneti kwamba wawakilishi wadi 17 pamoja naye hawakupigia kura hoja ya kumbandua madarakani Gavana Mutai.

Kiplagat alisema yeye na wenzake hawakuwa na imani na mfumo wa kielektroniki wa kupiga kura ambao uliletwa kwao saa chache tu kabla ya mjadala wa hoja hiyo.

Anasema kwamba ni wawakilishi wadi 29 kati ya wote 47 walipiga kura siku hiyo, kiwango kisichoakidi idadi hitajika ya thuluthi mbili ambayo ni sawa na wawakilishi wadi 32.

Kiplagat alidai kwamba Spika alikataa ombi lao la kutumia njia ya kitamaduni ya kupiga kura kwa kuitwa majina jambo lililowafanya wajizuie kupiga kura.

Alisema mfumo wa kielektroniki ulianzishwa bila mafunzo ya awali, miongozo wala mawasiliano kwa wanachama, hali iliyozua hofu ya udanganyifu wa kura.

Hata hivyo, Bunge la Kaunti liliwasilisha rekodi za kidijitali zilizoonyesha kuwa Kiplagat kwa kweli alipiga kura kuunga mkono hoja ya kumng’atua Mutai mamlakani.

Alikanusha hilo, akidai mtu fulani alijifanya kuwa yeye akaafikia mfumo huo bila idhini yake. Alifichua kuwa yeye na wawakilishi wadi 17 waliwasilisha malalamiko rasmi kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhusu suala hilo.

Wakili wa Bunge, Elias Mutuma, alimkashifu Kiplagat kwa kutokuwa mkweli, akitaja kumbukumbu za Hansard zinazoonyesha kuwa mwakilishi wadi huyo aliunga mkono ripoti ya kumng’atua Mutai.

Maseneta walieleza mashaka yao kuhusu uaminifu wa Kiplagat, hasa baada ya kukiri kuwa hakuingia bungeni na simu yake siku hiyo, kifaa muhimu kwa mfumo wa kupiga kura kwa njia ya kidijitali.

Maseneta walihoji umuhimu wa ushahidi wake, huku baadhi wakimtaja kuwa “shahidi mgumu.”

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa leo katika bunge la Seneti.

Share This Article