Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro amepokea tuzo ya heshima kama Gavana wa mwaka tuzo ya mabadiliko ya Utalii Kenya mwaka 2025 kutokana na umahiri na mchango wake mkubwa.
Mung’aro alipokea tuzo hiyo ya Tuzo za Jamhuri Kenya wakati wa sherehe za kuhitimisha awamu ya tatu la mashindano ya Gavana ya Gofu, ambayo alianzisha miaka mitatu iliyopita katika Klabu ya Gofu ya Malindi.
Wataalamu wa gofu na wachezaji wa kiwango cha kawaida wapatao 250 walihudhuria mashindano hayo ya siku mbili mwisho wa wiki, tukio lililochangia pakubwa katika kukuza utalii wa michezo.
William Onyango Odek kutoka Klabu ya Gofu ya Nyali aliibuka mshindi wa jumla wa Kombe la Gavana wa Kilifi na kujinyakulia zawadi kuu.
Kulikuwepo pia washindi wengine katika kundi la wachezaji wa gofu wa kiwango cha kawaida ambao walijinyakulia zawadi za pesa taslimu na zawadi nyinginezo.
Mung’aro alisema tuzo hiyo ni uthibitisho wazi kuwa juhudi za kufufua utalii zinaozaa matunda na akawahimiza wawekezaji wanaomiliki hoteli zilizo poromoka kuzijenga upya au kuziuza kwa wale walio tayari kuwekeza.
“Tamasha hili la kila mwaka linalodhaminiwa kwa fahari kupitia Taasisi yangu, linaendelea kuwaleta pamoja wachezaji wa golf, washirika na wadau katika jitihada za kukuza utalii wa michezo na kuitangaza Kilifi kama kitovu bora cha michezo,” alisema.
Alisema mashindano yajayo ya kila mwaka yatakuwa ya siku nne na mshindi atapokea zawadi ya shilingi milioni moja mwakani.
William Onyango Odek, mshindi wa jumla, alisema alifurahia ushindi na akamshukuru Gavana kwa kuandaa mashindano hayo ya golf.
Raymond Ngalla, CEC wa Kilifi anayesimamia Biashara, Utalii, Utamaduni, Urithi na Maendeleo ya Ushirika, alisema Kombe la Golf linaendelea kupata umaarufu na mipango inaendelea kulifanya kuwa kubwa zaidi na kuvutia wachezaji wa golf kutoka Kenya, Afrika Mashariki na ulimwenguni kote.