Gavana Kahiga wa Nyeri ashutumiwa vikali

Martin Mwanje
4 Min Read
Mutahi Kahiga - Gavana wa Nyeri

Gavana wa kaunti ya Nyeri Mutahi Kahiga ameendelea kushutumiwa vikali kutokana na matamshi yake yaliyoonekana kusherehekea kifo cha Waziri Mkuu wa zamani na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga. 

Kiongozi wa wengi katika Bunge la Taifa Kimani Ichung’wah ni miongoni mwa waliokuwa mstari wa mbele kumkosoa Gavana Kahiga kwa kutoa matamshi hayo ya kizembe.

“Kahiga, tutakuombea. Matamshi ya kizembe na kikatili kiasi gani? Nakosa maneno ya kukuambia lakini ikizingatiwa nilipatwa na msiba hivi karibuni, nafahamu kile ambacho naweza nikafanya sasa ni kukuombea mno,” alisema Ichung’wah ambaye pia ni mbunge wa eneo bunge la Kikuyu, kaunti ya Kiambu.

“Kukuombea kwamba Mwenyezi Mungu akupe hekima kiasi na kuomba kwamba hukuzungumza kwa niaba ya mkubwa wako kwa sababu waropokaji huonekana kurudia kile walichokisikia mkubwa wao akisema.”

Gavana wa kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru pia ameshtumu kauli za Kahiga akizitaja kuwa zisizofaa.

“Kauli zilizotolewa na mwenzangu, Gavana wa Nyeri siyo kwamba hazifai, zinakosa kuzingatia hisia za wengine na zinakosa uwajibikaji,” alisema Waiguru ambaye ameshutumiwa na upande wa upinzani kutoka eneo la Mlima Kenya katika siku za hivi karibuni.

“Kauli hizo haziakisi maoni ya uongozi au watu wa Mlima Kenya,” aliongeza Waiguru akisema eneo la Mlima Kenya linaungana na nchi nzima katika kumwomboleza Raila.

Mwingine aliyeshutumu matamshi ya Kahiga ni mwenyekiti wa chama tawala cha UDA Cecily Mbarire.

“Wakati ambapo taifa letu linaomboleza, taarifa kama hizo siyo tu za kizembe lakini zinazokosa heshima, siyo tu kwa kumbukumbu ya Mkenya shupavu bali pia kwa mamilioni ya Wakenya wanaoomboleza,” alisema Mbarire ambaye pia ni Gavana wa Embu.

“Wacha ieleweke vizuri: Kauli za Gavana Kahiga haziakisi maoni ya eneo la Mlima Kenya.”

Naibu kiongozi wa chama cha ODM ambaye pia ni Gavana wa Mombasa Abdullswamad Nassir hakuachwa nyuma katika kumlaani Gavana Kahiga.

“Chama cha ODM kinaelezea masikitiko yake makubwa na ghadhabu kutokana na matamshi ya kizembe, yenye kuleta migawanyiko na kufedhehesha yaliyotolewa na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga wakati wa tukio moja la umma huko Kieni – matamshi ambayo yalionekana kudhalilisha na hata kusherehekea kifo cha kiongozi wetu Raila Amolo Odinga, C.G.H,” alisema Nassir kwenye taarifa.

“Wakati ambapo mamilioni ya Wakenya bila kujali mirengo ya kisiasa, kikabila na kidini bado wanaomboleza, Gavana Kahiga aliamua kuongeza chumvi kwenye makovu ya wazi ya taifa.”

Licha ya matamshi hayo, Gavana Nassir alisema hawatayumba katika kuhubiri maadili ya umoja katika ujenzi wa taifa.

Katibu Mkuu wa ODM ambaye pia ni Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna kwenye taarifa amesema ingawa alifahamu kuna waliomchukia Raila, inashtua kwamba chuki hizo bado zinaendelea hata baada ya kifo chake.

“Mutahi Kahiga ndiye mwenye chuki zaidi kwenye kundi la waliomchukia, lakini Baba alitufunza daima kujibu chuki hizo kwa upendo. Kama angekuwa bado yuko hai, kile ambacho ungemwona akifanya ni kula chakula cha mchana na Kahiga.”

Baraza la Magavana limepanga mkutano wa dharura usiokuwa wa kawaida leo Jumatano asubuhi na kisha kuhutubia wanahabari kuhusiana na matamshi ya Kahiga.

 

 

Share This Article