Gavana Guyo: Rais Ruto hahusiki katika njama ya kunitimua madarakani

Martin Mwanje
3 Min Read
Abdi Guyo - Gavana wa Isiolo (mbele, kushoto)

Gavana wa kaunti ya Isiolo Abdi Ibrahim Guyo amekanusha vikali madai yanayosambazwa na wapinzani wake wa kisiasa kuwa Rais William Ruto ndiye anayehusika na mpango wa kumtimua madarakani.

Hii ni mara ya kwanza kwa Guyo kuzungumzia mpango huo wa Wawakilishi Wadi (MCAs) wa kumfurusha kwa njia ya hoja ya kumtimua madarakani.

Akihutubia maelfu ya wafuasi wake nje ya afisi yake jana Jumanne, Guyo aliwaonya wanaoeneza madai kuwa Rais Ruto anahusika na mchakato huo wasijaribu kulihusisha jina la Rais katika siasa za ndani za kaunti ya Isiolo.

Alisema tayari amezungumza na Rais mara mbili wiki hii na kwamba kiongozi huyo wa taifa alieleza wazi kuwa hajatoa agizo lolote la kutaka aondolewe afisini.

Guyo aliongeza kuwa kaunti ya Isiolo ni ngome ya kisiasa ya Rais Ruto na haipaswi kuvurugwa kwa sababu yoyote ile.

Alitaja kuwa MCAs 16 wanaounga mkono hoja ya kumtimua wamechochewa na wapinzani wake wa kisiasa kutoka nje ya mipaka ya Isiolo, lakini akaeleza kuwa yuko tayari kuzungumza nao ili kutatua changamoto zilizopo ili kuhakikisha ya kwamba utoaji huduma kwa wananchi hauathiriwi na mivutano ya kisiasa.

Mwakilishi Wadi ya Garbatula, Abdirashid Ali, ambaye pia ni kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Isiolo, aliitaja hatua ya Mwakilishi Wadi ya Sericho, Abubakar Godana, ya kuwasilisha hoja ya kumtimua Gavana Guyo kuwa ni kinyume cha sheria.

Alidai kuwa MCAs wanaotaka kumtimua Gavana huyo wanashirikiana na watu kutoka nje ya kaunti hiyo kuendeleza njama hiyo.

Abdirashid alisema kuwa watu wa Isiolo wana uwezo wa kutatua changamoto zao kwa njia ya mazungumzo na maridhiano bila kuingiliwa na watu kutoka nje.

Aliyekuwa mbunge wa Isiolo Kusini, Abdi Koropu Tepo, aliitaka Tume ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) kuchukua hatua dhidi ya mtu mmoja kutoka kaunti jirani ambaye inadaiwa alitoa matamshi ya uchochezi akidai kuwa kutakuwa na umwagikaji wa damu Isiolo, na kuyataja matamshi hayo kuwa ya kichochezi na hatari kwa amani ya umma.

Viongozi hao waliwataka MCAs kuheshimu amri ya muda iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Isiolo chini ya Jaji Nyaga Heston Mbogo, ambayo ilisitisha mchakato wa hoja ya kumtimua Gavana Guyo.

Vilevile, waliwataka wananchi kudumisha utulivu na kuendeleza mshikamano katika kipindi hiki cha mvutano wa kisiasa.

Kutokana na amri hiyo ya mahakama iliyotolewa siku mbili zilizopita, mikutano ya ukusanyaji maoni ya umma iliyokuwa imepangwa kufanyika leo Jumatano  katika wadi zote kumi ilifutwa rasmi na karani wa bunge la kaunti, Salad Boru, kupitia tangazo katika gazeti rasmi la serikali.

 

Share This Article