Gavana wa kaunti ya Isiolo, Abdi Ibrahim Guyo, amemshutumu vikali Seneta wa kaunti hiyo Fatuma Adan Dullo kufuatia matamshi aliyotoa bungeni kuhusu hali ya usalama Isiolo.
Guyo, aliyenusurika hoja ya kumbandua madarakani siku chache zilizopita, anamtuhumu Seneta Dullo kwa kugeuza visa vya uhalifu kuwa ajenda za kisiasa na kushambulia watumishi wa umma kama vile kamishna wa kaunti.
Akizungumza na wakazi wa Elsa Ntirim katika wadi ya Burat, katika shughuli yake ya kwanza ya kikazi tangu kunusurika kwake katika bunge la Seneti, Gavana Guyo aliwaonya viongozi wa kisiasa dhidi ya kutoa matamshi ya uchochezi yanayoweza kupandisha hasira miongoni mwa umma na kuhatarisha amani iliyopo kati ya jamii mbalimbali za Isiolo.
Guyo alieleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa tukio la kusikitisha la mama na watoto wake wanne kuchomwa moto wakiwa wamelala katika eneo la Bulapesa, lilitokana na mgogoro wa mapenzi, huku tukio jingine la kifo cha mwanablogu aliyefariki alipokuwa akipata matibabu katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) cha Hospitali ya Rufaa ya Isiolo, likisababishwa na ajali ya kugongwa na lori mjini Isiolo.
Aliwalaumu baadhi ya wanasiasa kwa kutumia matukio hayo kama silaha ya kisiasa, jambo linaloweza kuchochea hisia kali kwa wananchi.
Aidha, aliwataka viongozi wa kisiasa kukoma kutumia majukwaa ya bunge kuwashambulia maafisa wa serikali kama kamishna wa kaunti, ambao hawana fursa ya kujitetea bungeni.
Aliwaomba Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen na Katibu wake Dkt. Raymond Omollo kuwahakikishia usalama na ulinzi watendaji hao wa serikali wanapotekeleza majukumu yao.
Guyo alisisitiza kuwa masuala ya usalama yasiachwe mikononi mwa wanasiasa bali yaachwe kwa vyombo vya usalama.
Kuhusu jaribio la kumwondoa mamlakani, Gavana Guyo aliwaambia waliopanga njama hiyo kuwa hakuna njia ya mkato kufikia kiti cha ugavana, na kwamba muda wa uchaguzi ni mwaka wa 2027 ambapo yeyote mwenye nia ya kuwania kiti hicho anatakiwa kuomba ridhaa ya wananchi wa Isiolo.
Katika ziara hiyo, Guyo alikagua miradi miwili ya maji katika eneo la Elsa Ntirim iliyotekelezwa na serikali ya kaunti ya Isiolo kupitia Mpango wa Ufadhili wa Kijamii wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (FLOCCA).
Ni hatua iliyowapa motisha zaidi ya wakulima 100 kuongeza uzalishaji wa kilimo, na kufufua kwa mafanikio Mradi wa Unyunyiziaji Mashamba Maji wa Elsa Ntirim.