Gavana Barasa azindua ujenzi wa soko la Likuyani

Dismas Otuke
1 Min Read

Gavana wa kaunti ya kakamega Fernandes Barasa hii leo Jumanne adhuhuri amezindua rasmi ujenzi wa soko la Likuyani.

Soko hilo lenye nafasi 300, litajengwa kwa ushirikiano wa serikali ya kaunti hiyo na serikali ya kitaifa chini ya uongozi wa Rais William Ruto, kwa lengo la kuboresha biashara na uchumi wa wakazi wa eneo hilo.

Kwenye hotuba yake, Barasa alisema kuwa kando na soko hilo, serikali yake na ile ya kitaifa zinashirikiana kujenga hifadhi ya viwanda katika eneo hilo kwa gharama ya shilingi milioni 500.

Eneo hilo litatumiwa kwa shughuli za kuongeza thamani ya bidhaa na hivyo kubuni nafasi za ajira na kustawisha biashara. Katika mpango huo, serikali yake itachangia milioni 250.

Zaidi ya hayo, alifichua kuwa serikali yake ina mpango wa ujenzi wa kiwanda cha nguo katika eneo hilo.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Naibu Gavana Ayub Savula, mbunge wa Likuyani Innocent Mugabe, wawakilishi wadi, wafanyabiashara na wakazi.

Share This Article