Kaunti ya Nyandarua imechukua hatua muhimu ya kupunguza gharama za miundombinu na kuharakisha maendeleo ya kisasa kwa kuzindua rasmi kiwanda cha kutengeneza kabro kwa wingi cha Ol’Kalou, kilichoko katika Wadi ya Kaimbaga.
Kiwanda hicho, kilichozinduliwa na Gavana Dkt. Moses Kiarie Badilisha, kinatarajiwa kupunguza gharama za kutengeneza barabara za kabro katika miradi ya umma kwa zaidi ya asilimia 60.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Gavana Badilisha alisisitiza kuwa kiwanda hicho kitakuwa na mchango mkubwa katika ajenda ya kisasa ya kaunti, inayolenga zaidi ya miji mikuu kumi na taasisi nyingi za huduma kwa umma.
“Uzinduzi wa kiwanda hiki si tu kwamba utaongeza nafasi za ajira kwa vijana wetu, bali pia utaharakisha mchakato wa kuendeleza miji yetu kuwa ya kisasa. Baada ya miji kuu kuboreshwa, tunapanga kutoa huduma za cabro kwa raia binafsi kwa bei nafuu ili kuongeza mapato ya kaunti,” alisema Badilisha.

Katika hotuba tofauti wakati wa ziara ya kukagua miradi inayoendelea katika mtaa wa Huruma, Wadi ya Kaimbaga, Gavana alisisitiza tena dhamira yake ya kubadilisha makazi yote — rasmi na yasiyo rasmi — kuwa mazingira bora ya kuishi yanayowezesha biashara ndogo na kubwa kustawi.
Mtaa wa Huruma, ambao awali ulianzishwa kama makazi ya kihistoria ya kikoloni, unafanyiwa ukarabati mkubwa. Maboresho hayo yanajumuisha barabara mpya zilizotengenezwa kwa kabro, usakinishaji wa mfumo wa kisasa wa maji taka, soko jipya la rejareja litakalohudumia wafanyabiashara zaidi ya 200, pamoja na taa za barabarani zinazotumia nishati ya jua — yote haya yakiwa sehemu ya mradi wenye thamani ya zaidi ya shilingi miioni 200.
Maboresho haya yako chini ya Mpango wa Uboreshaji wa Makazi Yasiyo Rasmi nchini Kenya (KISP), ambao pia unajumuisha uboreshaji wa kijiji cha Gichagi katika Wadi ya Njabini-Kiburu. Mradi huu pacha, wenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 400, utanufaisha zaidi ya kaya 700 na kutoa huduma sawa za miundombinu.