Gavana wa Kwale Fatuma Achani amezindua rasmi ujenzi wa jengo la huduma za dharura kwenye hospitali ya rufaa ya Mwambweni huko Msambweni.
Ujenzi wa kituo hicho, kwa ushirikiano wa serikali ya kaunti ya Kwale na shirika la Emergency Medicine Kenya Foundation, unalenga kupunguza idadi ya watu wanaopoteza maisha wanapohusika na ajali mbalimbali zikiwemo za barabarani, pamoja na ukosefu wa huduma nyingine za dharura.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Gavana Fatuma Achani amesema kuwa ujenzi wa kituo hicho, mbali na kupeana huduma za dharura, pia utasaidia kuboresha huduma za afya kwenye hospitali ya rufaa ya Msambweni kwa wakazi wa eneo hilo na kaunti ya Kwale kwa ujumla.
Hadi sasa, kaunti ya Kwale imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Hospitali ya Rufaa ya Msambweni, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa Kitengo cha Wagonjwa Mahututi (ICU), Kitengo cha Wagonjwa wa Figo, Kitengo cha Watoto Wachanga, kiwanda cha kutengeneza oksijeni, jumba la kuhifadhia dawa, mtambo wa kutibu maji, pamoja na wodi mpya ya kina mama kujifungua yenye vitanda 60.
Kwa upande wake, meneja wa shirika la Emergency Medicine Kenya Foundation Lilian Waihuini, amesema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali ya kaunti ya Kwale ili kuhakikisha visa vya upotezaji wa maisha kutokana na ajali vinapungua katika kaunti hiyo.
Ni kauli iliyoungwa mkono na Naibu Gavana wa kaunti hiyo Josphat Chirema Kombo.
Wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na Suleiman Koi, wameutaja mradi huo kama hatua mojawapo ya kudhibiti vifo vya watu vilivyokuwa vikishuhudiwa awali kutokana na ukosefu wa huduma hizo.