Gavana Achani azindua Greda mbili za kuboresha barabara Kwale

Marion Bosire
2 Min Read

Gavana wa Kwale Fatuma Achani, amezindua rasmi mashine mbili mpya za kutengeneza barabara, zitakazotumiwa kuboresha barabara na miundombinu katika maeneo ya vijijini kote katika kaunti hiyo.

Kufikia sasa, serikali ya Kaunti ya Kwale imenunua mashine sita za kutengeneza barabara, imeweka murram kwenye barabara za urefu wa kilomita 1,688 kwa jumla, imeweka lami kilomita 15.22 za barabara mpya na kujenga daraja moja.

Baadhi ya barabara zilizoboreshwa ni barabara ya kutoka Tiwi hadi Vinuni iliyowekwa lami, ile ya kutoka Kona ya Polisi hadi Hospitali ya Msambweni, ya kutoka Tsimba hadi Mbuguni na ile ya kutoka Mangwei hadi Majoreni.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi katika Makao Makuu ya Kaunti ya Kwale, Gavana Achani alisema mashine hizo mpya zitapelekwa katika maeneo mbalimbali ya kaunti kusaidia katika matengenezo ya barabara na kufungua barabara mpya za vijijini.

“Greda hizi zitatusaidia kufungua maeneo ambayo hayawezi kufikika, hasa wakati wa mvua, ili kurahisisha usafiri,” alisema Gavana Achani.

Aliongeza kuwa mitandao bora ya barabara ni muhimu katika kufanikisha uwezeshaji wa kiuchumi, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na elimu na kuongeza uzalishaji wa kilimo.

Rashid Mwamaneno, mkazi wa eneo hilo, alimshukuru gavana kwa mashine hizo, akisema hali mbaya ya barabara imekuwa kikwazo kikubwa kwa usafiri na maendeleo kwa muda mrefu.

“Tumeteseka kwa miaka mingi, hasa wakati wa mvua. Mashine hizi ni afueni kubwa. Tunatumaini barabara zetu sasa zitapitika,” alisema.

Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kaunti ya Kwale, Tumaini Mwachaunga, aliipongeza serikali ya kaunti kwa kuwekeza katika miundombinu, akibainisha kuwa uwekezaji huo unaathiri maisha ya wananchi moja kwa moja maisha ya wananchi.

Alitaja usafirishaji wa mazao sokoni na hatua ya kuhakikisha magari ya wagonjwa yanaweza kufika maeneo ya ndani bila kuchelewa.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Barabara wa kaunti ya Kwale Ali Joto, Waziri wa Elimu Mishi Kaole na viongozi wengine.

Share This Article