Gavana Achani awahimiza wakazi wa Kwale kupanda miti

Tom Mathinji
2 Min Read
Gavana wa Kwale Fatuma Achani.

Gavana wa Kwale Fatuma Achani, ametoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo hususan wale wanaoishi katika maeneo kame kama vile  Kinango, Samburu, na Lungalunga, kupanda miti, kama njia ya kukabiliana na hali ya kiangazi ambayo hughubika maeneo hayo.

Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Ganze, eneo bunge la Matuga, Achani alisisitiza haja ya ushirikiano kati ya serikali ya kaunti hiyo na wakazi wa eneo hilo katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi, na kutafuta suluhu la kudumu la ukosefu wa maji.

“Ili kukabiliana na ukosefu wa maji unaokumba sehemu kadhaa za kaunti hii, lazima tupande miti zaidi. Nawahimiza kuchukua jukumu la kuhifadhi ardhi yetu,” alisema Gavana Achani.

Aidha Gavana huyo aliongoza shughuli ya upanzi wa miche 10,000 ikiwemo ya miembe, ile ya Casuarina na arborea.

Achani alidokeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa bwawa la Ganze unaojumuisha sehemu za kunywesha mifugo maji, maduka ya kuuzia maji na usambazaji wa miche, ni baadhi ya juhudu za serikali yake kwa lengo la kutokomeza athari za kiangazi katika kaunti hiyo.

“Utawala wangu umejitolea kuhakikisha unakabiliana na  swla la kiangazi kikamilifu,” aliongeza Achani.

Kwa muda wa miaka mingi maeneo ya Kinango, Samburu na LungaLunga, yamekuwa yakitegemea chakula cha msaada kutokana na hali ya kiangazi ambayo imeathiri shughuli za kilimo katika maeneo hayo.

Ili kukabiliaana na hali hiyo, serikali ya kaunti ya Kwale ilijenga mabwawa 20 ambayo hutoa maji ya kutosha kwa matumizi ya nyumbani, kunyunyizia mashamba na kuwapa mifugo.

Mabwawa hayo ni pamoja na Nyalani( Wadi ya Kinango), Nuru (Puma), bwawa la Mtaa (Mwavumbo), bwawa la Mwakalanga (Mwereni), Chikwakwani ( Kasemeni)na bwawa la  Bang’a (Kaunti ndogo ya Kinango).

Share This Article