Gavana wa Kwale Fatuma Achani ameanzisha mradi wa kilimo nyunyizi wa shilingi milioni 2.6, utakaomilikiwa na kikundi cha Dzipange Kayamba Self Help Group, wadi ya Tiwi katika eneo bunge la Matuga ili kupiga jeki wakulima wadogowadogo kupata mazao bora na kuwe na chakula toshelevu kwa jamii.
Akizungumza na wakulima hao, Achani amewahimiza kujiunga katika vyama vya akiba na mikopo ili waweze kupata mtaji mkubwa utakaowasaidia zaidi katika kufanya shughuli za ukulima akiwaahidi kuwa soko la mazao yao litapatikana.
Kwa upande wa wakulima wakiongozwa na Salim Golo, amewataka wakulima wenza wa Kwale kuweza kukumbatia kilimo ili kukabili uhaba wa chakula uliokuwa ukikumba kaunti hiyo mara kwa mara.
Serikali hiyo ya Kwale imeweza kuchimba zaidi ya mabwawa 40, hasa katika maeneo kame, ili kuweza kuendeleza kilimo cha umwagiliaji pamoja na kunusuru mifugo wakati wa kiangazi.