Mtangazaji wa Uganda Jennifer Nakanguubi maarufu kama Full Figure yuko katika hatari ya kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na kiwango cha chini cha watu waliojitokeza kuhudhuria tamasha la Alien Skin.
Mwandalizi wa matamasha Nobat Twizire mmiliki wa kampuni ya Nobat Events ametangaza nia ya kumchukulia Full Figure hatua za kisheria kutokana na usemi wake ambao anadai ulisababisha hali hiyo.
Mwanamuziki Alien Skin alikua na tamasha katika eneo la Lugogo Cricket Oval Februari 21, 2025, ambalo halikufanikiwa kuvutia watu wengi kama ilivyotarajiwa.
Kulingana na Twizire Full Figure alishtua watu ambao wangetaka kuhudhuria tamasha hilo pale aliposema kwamba lingejaa visa vya wizi na dhuluma.
“Kama unataka kupigwa nenda Cricket Oval. Kama unataka kubakwa, kama unajaribu kupoteza simu yako au kung’olewa jicho nenda tu kwenye hilo tamasha la Lugogo” ndiyo maneno aliyoyasema Full Figure, kulingana na Twizire.
Mwandalizi huyo wa matamasha anasema atadai fidia ya shilingi milioni 250, pesa za Uganda katika kesi atakayowasilisha dhidi ya Full Figure.
Usemi wa Full Figure kulingana naye, ulilenga kuhujumu tamasha lao na kujaza watu ambao wangependa kuhudhuria woga ili wasiende.
Twizire alikiri kwamba kulikuwa na watu kadhaa kwenye tamasha hilo ambao walinunua tiketi za kawaida na ni wapenzi wa Alien Skin lakini wateja ambao wangenunua tiketi ghali hawakujitokeza.
Alisema baadhi ya wateja ambao walikuwa tayari wamenunua tiketi hizo ghali waliomba warudishiwe pesa zao kwani walikuwa na shaka kutokana na yale ambayo walikuwa wamesikia.