Mwanamuziki wa Uganda ambaye pia ni mhamasishaji wa chama tawala nchini humo NRM, Jennifer Nakaguubi maarufu kama Full Figure, hatimaye amezungumzia tukio la kushambuliwa.
Full Figure amethibitisha kuwa ni kweli ndiye aliyekuwa kwenye vipande vya video vilivyosambaa sana mitandaoni.
Kulingana na video zilizosambaa tarehe 31 Agosti, Full Figure alishambuliwa na wanaume wawili waliompiga vibaya, na kusababisha alazwe hospitalini akiwa na majeraha usoni.
Watu kadhaa wametajwa kuhusika na kupanga shambulio hilo, wakiwemo mahasimu wake wa muda mrefu kama Justine Nameere, ambaye baadaye alikanusha tuhuma hizo hadharani.
Katika mahojiano Full Figure alieleza kuwa ni kweli alishambuliwa na kwamba uchunguzi unaendelea kufanywa na polisi ili kuwakamata wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Aidha, mwanadada huyo mwenye kauli kali alisema kuwa waliomshambulia walikuwa wakitafuta umaarufu na kutajwa kwenye vyombo vya habari.
“Sijawahi kumshambulia mtu ambaye hajaanza ugomvi. Wananishambulia kwa ajili ya kutafuta umaarufu; wengine wamefungua chaneli na hupata umaarufu na watazamaji wengi wanaponizungumzia.” alielezea mwanadada huyo.
Aliongeza kusema kwamba yeye ndiye chanzo cha mapato ya watu kama hao, lakini wanamtumia vibaya na kwamba watu ambao huwa tunakaa karibu nao muda mrefu ndio hutuumiza zaidi.
Haya yanajiri wakati ambapo kampeni na shughuli nyingine za kisiasa zinaendelea kushika moto nchini Uganda kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Januari mwakani.