Shirika la Utangazaji nchini, KBC lina Kaimu Mkurugenzi Mkuu mpya.
Hii ni baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo ikiongozwa na mwenyekiti wake Tom Mshindi leo Jumatatu kumteua Florence Migunde kukaimu wadhifa huo.
Migunde anachukua wadhifa ulioachwa wazi na Paul Macharia ambaye muda wake wa kukaimu wadhifa huo ulikamilika Alhamisi iliyopita, Septemba 19, 2024.
“Ili kuhakikisha shughuli za KBC zinaendelea vyema, Bodi ya Wakurugenzi, baada ya kutafakari imemteua Bi. Florence Migunde kuwa Kaimu Mkurugenzi kuanzia leo Jumatatu, Septemba, 2024 hadi Mkurugenzi Mkuu atakapoteuliwa,” alisema Mshindi katika taarifa.
“Wafanyakazi wote wanatakiwa kumuunga mkono kikamilifu na kumpa ushirikiano Kaimu Mkurugenzi Mkuu ili kuhakikisha utoaji bora wa huduma.”
Kwa sasa, Migunde anahudumu kama Meneja wa Masoko wa KBC.
Mnamo mwezi Mei Mwaka huu, Agnes Kalekye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa KBC.
Hata hivyo, Mahakama Kuu ilisitisha uteuzi wa Kalekye na watu wengine watatu walioteuliwa kuhudumu katika mashirika mbalimbali serikalini.
Hii ni baada ya kesi kuwasilishwa na Daktari Magare Gikenyi mjini Nakuru kupinga uteuzi wao akidai ulifanywa kwa mashauriano na Mkuu wa Utumishi wa Umma wakati sheria inaelezea kuwa unapaswa kufanywa na Rais.
Uamuzi wa kesi hiyo bado unasubiriwa.