Flaqo asema utajiri wa kweli haujionyeshi

Alisema matajiri wa ukweli hawana haja ya kujionyesha akisisitiza kwamba utajiri wa ukweli mara nyingi huwa wa kimya kimya.

Marion Bosire
1 Min Read

Flaqo Raz ambaye ni mtengeneza maudhui mitandaoni nchini Kenya amesema kwamba utajiri wa kweli sio wa kujionyesha.

Alikuwa akizungumza kwenye mahijiano ambapo alisema kwamba matajiri wa ukweli huwa hawana haja ya kujionyesha akisisitiza kwamba utajiri wa ukweli mara nyingi huwa wa kimya kimya.

Mwigizaji huyo ambaye aliwakwaza wanaojihusisha na biashara ya ubadilishanaji wa sarafu almaarufu Forex Trading alisema kwamba watu ambao wana mali nyingi wanaishi maisha ya kawaida na huwa hawajitakii makubwa kwa kuonyesha wanachomiliki.

“Sio lazima utangaze, Nina pesa, naendesha gari fulani, ninamiliki GLE” alisema Flaqo kwenye mahojiano hayo akitoa mfano wa mmiliki wa duka la bidhaa za ujenzi.

Kulingana naye, watu kama hao huwa na pesa nyingi kwenye akaunti zao za benki lakini huwa hawatangazi kwamba wanazo kwa kununua vitu ghali vya starehe.

Alizungumzia wale ambao huwa wanahisi ni lazima waonyeshe mali zao na hata nguo ghali wanazovaa akisema nia yao ni kuonyesha ukubwa wao.

Msanii huyo anaamini kwamba utajiri ni hali ya kimawazo ambayo inapendelea sana uthabiti na uhuru na wala sio kuonyesha mali zako mara kwa mara.

Flaqo alifichua kwamba ana uwezo wa kununua gari kubwa lakini amechagua kutolinunua kwa ajili ya kujionyesha tu na kudhihirisha uwezo wake kifedha.

Share This Article