Fid Q afunguka sababu ya kuchelewa kuoa

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Tanzania Farid Kubanda maarufu kama Fid Q amezungumzia kuhusu maisha yake na sababu yake ya kuchelewa kuoa kwa mara ya kwanza.

Fid Q ambaye huimba nyimbo za mtindo wa Hip Hop alizungumza kwenye mahojiano ambapo alisema kwamba kuchelewa kwake kuingia kwenye ndoa hakukuwa kwa bahati mbaya bali kulikuwa na sababu kubwa ya kutopata mwanamke sahihi mapema.

“Nilichelewa kuoa kwa sababu nilichelewa kupata mwanamke ambaye tungeendana, kwani ambao nilikuwa nawapata tulikuwa hatuendani baadhi ya vitu” alisema msanii huyo.

Alisema alivyompata mke wake aliona kwamba kuna vitu vingi ambavyo wanashabihana huku tofauti zao zikiwa chache.

Fid Q anaonekana kuwa na furaha kubwa na ndoa yake, kwani mwaka huu anatimiza miaka tisa tangu afunge ndoa na kipenzi chake, anayemuita kwa upendo Mama Cheusi.

Mashabiki wake mitandaoni wamepongeza ujasiri wake wa kuzungumzia maisha yake ya ndoa hadharani na wamemtakia maisha marefu yenye upendo na furaha zaidi.

Share This Article