Rais William Ruto amewapongeza Wakenya walio Ughaibuni kwa kuimarisha mchango wao kwa maendeleo ya taifa, akidokeza kuwa fedha zinazotumwa na Wakenya walio nje ya nchi zimeongezeka katika muda wa miaka miwili iliyopita.
Akizungumza alipokutana na wawakilishi wa Wakenya wanaoishi nje ya nchi katika Ikulu ya Nairobi, kiongozi wa taifa alielezea haja ya kuboresha ujuzi na rasimali za ughaibuni kupitia sera zilizoratibiwa vyema.
“Tunapongeza mchango unaotekelezwa na Wakenya wanaoishi na kufanya kazi ughaibuni,kwa maendeleo ya taifa hili,” alisema Rais Ruto.
Kulingana na Rais Ruto, fedha zinazotumwa hapa nchini zimeongezeka kutoka shilingi bilioni 516 hadi shilingi bilioni 638 mwaka 2023.
“Tunatambua fedha zinazotumwa kutoka ughaibuni na jukumu muhimu zinatokeleza katika kupiga jeki familia na jamii, uwekezaji na kuimarisha akiba yetu ya fedha za kigeni ambayo kwa sasa ni dola bilioni 10.8,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi wa taifa alidokeza kuwa wakenya 393,000 wamepata ajira katika mataifa ya kigeni katika muda wa miezi 16 iliyopita, kama sehemu ya juhudi za serikali za kupanua fursa za ajira.