Ethiopia kutumia bandari ya Lamu baada ya makubaliano na Kenya

Tom Mathinji
2 Min Read
Ethiopia kuanza kutumia bandari ya Lamu.

Bandari ya Lamu inatarajiwa kuwa na shughuli nyingi, kufuatia makubaliano kati ya Kenya na mataifa jirani, kuitumia kama kitovu cha uchukuzi wa baharini.

Alipozuru eneo hilo leo Alhamisi, Rais William Ruto alitangaza makubaliano mapya baina ya Kenya na Ethiopia ya kusafirisha mizigo kutoka bandari hiyo hadi nchini Ethiopia.

“Tumekubaliana na serikali ya Ethiopia ianze kutumia bandari ya Lamu, ili tuweze kubuni nafasi zaidi za ajira na kukuza uchumi wa kanda hii,” alisema Rais Ruto.

Kiongozi wa taifa alisema hivi karibuni ataandaa mkutano wa viongozi wa kanda hii katika bandari ya Lamu, ambayo ndiyo ya pili kwa ukubwa baada ya ile ya Mombasa.

Kiongozi wa taifa alisema hayo alipozindua mradi mkuu wa nishati ya jua wa kisiwa cha Ndau, eneo bunge la Lamu mashariki, kaunti ya Lamu.

Wakati uo huo, Rais Ruto alitangaza kwamba vituo vitatu vya kwanza vya kisasa vya kupakulia meli katika bandari ya Lamu, vimekamilika na viko tayari kutumiwa.

Aidha alisema serikali imetenga shilingi bilioni 1.7 ili kuwafidia wavuvi waliohamishwa ili kutoa fursa ya ujenzi wa bandari hiyo.

Bandari ya Lamu ni sehemu muhimu ya miundo mbinu ya uchukuzi baina ya bandari ya Lamu, Sudan kusini na Ethiopia yaani Lapsset, ambao umekuwa ukijengwa tangu mwaka  2012.

Share This Article