Ethekon: Tutatekeleza majukumu yetu kwa dhati

Martin Mwanje
2 Min Read
Erastus Edung Ethekon - Mwenyekiti mpya wa IEBC

Mwenyekiti mpya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Erastus Edung Ethekon amewaahidi Wakenya kuwa atajizatiti kuhakikisha tume hiyo inawatumikia kwa dhati. 

Aidha, ameahidi kuwa uaminifu wake wa kwanza utakuwa kwa Wakenya.

Hata hivyo, ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo, alitoa wito kwa washikadau wote na Wakenya kwa jumla kushirikiana nao kwa bega kwa bega kufanikisha utenda kazi wa tume hiyo.

“Kwa heshima kubwa na unyenyekevu nachukua hatamu za uenyekiti wa IEBC, taasisi ambayo ni kiini cha demokrasia. Uamiminifu wangu wa kwanza ni kwa Wakenya. Ningependa kuwahakikishia Wakenya kwamba sauti zao zitasikika na kuhesabika katika chaguzi zijazo. Tunawasihi kutuunga mkono katika safari hii ya mamlaka shirikishi,” Ethekon alitoa rai katika hotuba yake ya kwanza baada ya kula kiapo cha utenda kazi katika majengo ya Mahakama ya Juu.

“Tunapochukua hatamu kama tume mpya ya IEBC, natoa wito kwa taasisi zingine na washikadau kutuunga mkono na kufanya kazi kwa pamoja  ili kuhakikisha hata tunapofanya mipango ya chaguzi ndogo na uchaguzi mkuu jao, tunatekeleza mamlaka yetu kuhakikisha michakato ya uchaguzi wa amani, kuaminika na kuwajibika.”

Wengine walioapishwa kama Makamishna wapya wa IEBC ni aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Aduol na Fahima Araphat Abdallah.

Wote hao watahudumu kwa kipindi kisichozidi miaka 6 kuanzisa siku ya uapisho.

Share This Article