Ethekon: Sitapendelea upande wowote wakati wa Uchaguzi Mkuu 2027

Tom Mathinji
1 Min Read
Erastus Edung Ethekon.

Erastus Ethekon ambaye ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), amesema atashikilia uhuru wa tume hiyo na atafanikisha uchaguzi wa kuaminika mwaka 2027.

Alipofika mbele ya kamati ya Bunge la Taifa kuhusu Haki na Maswala ya Sheria (JLAC) leo Jumamosi, Ethekon alisema ataongozwa na katiba ya Kenya atakapokuwa akitekeleza majukumu yake.

“Sitapendelea upande wowote,” alithibitisha Ethekon.

“Nitaongozwa na sheria za taifa hili, nitafuata michakato yote iliyowekwa itakayotuelekeza kwa uchaguzi wa kuaminika,’ aliongeza mwenyekiti huyo mteule.

Aidha, alikanusha kuwa uhusiano wowote na aliyekuwa Gavana wa Turkana ambaye sasa ni Naibu Mkuu wa Wafanyakazi katika Ikulu ya Rais, Josphat Nanok.

Ethekon, aliyekuwa mshauri wa kisheria wa Nanok alipokuwa Gavana wa Turkana, aliambia kamati hiyo kuwa uhusiano wake wa kikazi wa awali na Nanok, hautaingilia kwa vyovyote jukumu lake katika tume ya IEBC.

“Sina uhusiano wowote na Mheshimiwa Nanok. Hatuna uhusiano wa kuzaliwa au wa Kikoo,” alithibitisha Nanok.

Ethekon, ambaye ni mwanasheria, alikiri kuwepo kwa changamoto katika mchakato wa uchaguzi wa tafa hili, lakini alisema atajizatiti kukabiliana nazo iwapo ataidhinishwa kwenye wadhifa huo.

Share This Article