Ero Kamano William, Raila Junior amshukuru Rais Ruto

Marion Bosire
1 Min Read

Mwana wa kiume wa aliyekuwa waziri mkuu Raila Amolo Odinga. Raila Odinga Junior, amemshukuru Rais William Ruto kwa usaidizi wake wa maandalizi ya mazishi ya kitaifa ya babake mzazi.

Akizungumza wakati wa hafla ya mazishi ya babake katika chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Jaramohi Oginga Odinga, Junior alisema amesafiri na mwili wa babake tangu alipoaga dunia na hivyo anashukuru Rais kwa usaidizi huo.

Raila Junior aliongoza umati wa waombolezaji katika kufoka maneno “Ero Kamano William” yaani “Asante sana William kabla ya kuendeleza hotuba yake.

Katika hotuba yake, Junior alitambua viongozi wote waliosimama na familia yao wakati huu mgumu akitoa shukrani za dhati.

Mwana huyo wa mwendazake alitambua watu wa familia yake akitaja marehemu Fidel, Dadake Rosemary na kitindamimba Winnie Odinga.

Kijana huyo alisimamisha hotuba yake kwa muda kutambua mkewe hata ingawa hakumpa nafasi ya kuzungumza huku akiorodhesha majina ya wajukuu wa babake.

Alitambua pia wote waliokuwa wakifanya kazi na babake ambapo alisema kwamba hangeweza kutambua wote kwa majina lakini hakusahau kumtaja mlinzi wake wa kibinafsi Bwana Ogeta.

Junior aliongoza pia umati kuimba wimbo mkuu wa timu ya soka ya Gor Mahia ambayo babake alikuwa akiongoza kama mlezi.

Share This Article