Emmanuella akanusha uvumi unaoenezwa kumhusu

Mchekeshaji huyo wa umri wa miaka 15 anasema mambo yote ambayo yamesemwa kumhusu mitandaoni sio ya kweli.

Marion Bosire
1 Min Read

Mchekeshaji na mwigizaji wa Nigeria Emmanuella Samuel maarufu kama Ella, amezungumzia uvumi ambao umekuwa ukienezwa mitandaoni kumhusu.

Ella wa umri wa miaka 15 sasa alikuwa akizungumza kwenye mahojiano ambapo aliangazia uvumi kama wa kuolewa na kuwa mjamzito ilhali yeye ni mtoto.

“Kuna maneno mengi yanasemwa kunihusu. Nimesikia mengi, lakini ninajua ukweli. Kuna moja ilisema mimi ni mjamzito, kwamba nimeolewa, yote hayo sio ya kweli.” Alisema Ella.

Alielezea kwamba uvumi huo hauna ukweli wowote isipokuwa dai moja la kujengea wazazi wake nyumba akiwa na umri wa miaka 10 pekee.

Hatua ya kujengea wazazi wake anasema ilitokana na upendo alionao na anajali familia yake ndiposa akataka kuondolea wazazi wake mzigo wa kulipa kodi ya nyumba.

Emmanuella ndiye mtoto wa nne kati ya watoto wote sita wa wazazi wake na anasisitiza kwamba hakushurutishwa kujengea wazazi wake bali alifanya uamuzi binafsi.

“Nilihisi kwamba haikuwa sawa kwa mamangu kuendelea kuishi kwenye nyumba ya kupangisha nikapata wazo la kuwajengea eneo ambalo hawangehitajika kulipa kodi.” alisema binti huyo.

Emmanuella alijipatia umaarufu baada ya kuigiza kwenye video za vichekesho za Mark Angel Comedy akiwa na umri mdogo.

Share This Article