Emmanuel Bwiire mwanamuziki wa Uganda na mmoja wa wanachama wawili wa kundi la muziki la Benti Boys, ametoweka, haya ni kulingana na mwimbaji mwenzake Steven.
Steven alifichua hayo alipokuwa akihojiwa kwenye kituo kimoja cha runinga nchini humo ambapo walidhihirisha wasiwasi kuhusu usalama wa mwenzake.
Kulingana na Steven, simu ya Bwiire ilikuwa haiingii tangu jana alasiri alipoondoka kwenye makazi yao ya pamoja akitumia gari yake na hawajawasiliana tangu wakati huo.
Wawili hao walikuwa pamoja juzi usiku kwenye studio za Temperature Touch kabla ya kutumbuiza katika eneo la Pier One.
Steven anasema kutoweka kwa Bwiire sio jambo la kawaida akisisitiza kwamba wamezoea kujuliana hali kila mara na kufahamishana wanakokwenda.
“Simu za Emmanuel zimezimwa tangu jana saa nane mchana. Aliondoka akitumia gari na hapatikani kwenye simu” alielezea Steven kwenye mahojiano ya leo.
Hata hivyo Steven amekanusha dhana kwamba huenda kutoweka kwa mwenzake kunahusiana na siasa akifafanua kwamba hajawahi kujihusisha na chama chochote cha kisiasa.
Steven sasa anaomba yeyote aliye na habari zinazoweza kusaidia katika kumpata Emmanuel ajitokeze na kusaidia kumtafuta.
Kulingana na maelezo kwenye akaunti yao ya YouTube, Benti Boys Afrika ni kundi la muziki linalohusisha kaka wawili, ambao nyimbo zao ni za mitindo ya dancehall na afrobeat.