Msanii wa muziki nchini Marekani Eminem ameshtaki kampuni ya mitandao ya kijamii Meta kwa kile anachokitaja kuwa hatua ya kuwezesha ukiukaji wa hakimiliki ya kazi zake za muziki.
Kampuni inayosimamia usambazaji wa kazi za msanii huyo Eight Mile Style inadai fidia ya Yuro milioni 80.6 kutoka kwa Meta ikisema kwamba za Eminem 243 zilitumika kwenye majukwaa kadhaa ya Meta bila idhini.
Katika kesi hiyo, Eminem na kampuni hiyo wanadai kwamba Meta, inayomiliki mitandao ya kijamii ya Facebook, Instagram na WhatsApp ilikubalia watumizi kuchapisha video fupi walizorekodi na kuambatanisha na nyimbo zake.
Kulingana na kesi hiyo, makosa hayo yalifanyika kukiwepo na leseni na hivyo kudunisha hakimiliki ya msanii huyo.
Mawakili wa Eminem wanadai kwamba kampuni ya Meta ilifaidi kutokana na ukiukaji huo wa hakimiliki yake badala ya kuhakikisha kwamba inalindwa.
Iwapo hawataafikia makubaliano kuhusu fidia, msanii huyo ataitisha malipo ya dola elfu 150 kwa kila wimbo uliotumika pesa ambazo zitakuwa dola milioni 109 kwa jumla.
Hii sio mara ya kwanza kampuni ya Meta inajipata katika hali hii, mwaka 2022 kampuni ya Epidemic Sound, ilidai kwamba kulikuwa na matumizi yasoidhinishwa ya miziki yake kwenye mitandao ya kijamii ya Meta.