Tume inayoshughulikia makosa ya kiuchumi na kifedha nchini Nigeria EFCC imetangaza kwamba imemwachilia huru mwanamitandao Martins Innocent Otse maarufu kama VeryDarkMan au VDM.
Huku ikielezea kwamba VDM ameachiliwa kwa dhamana, EFCC ilielezea kwamba alikamatwa kufuatia hatua yake ya kususia mialiko yao kuhusu masuala mbali mbali.
Masuala hayo yanajumuisha uhalifu wa kifedha kulingana na EFCC.
VDM alikamatwa na maafisa wa EFCC Ijumaa nje ya benki ya GTB jijini Abuja nchini Nigeria, tukio lililozua mjadala mkali mitandaoni huku wengi wakitaka aachiliwe huru.
Mawakili wa VDM wakiongozwa na Deji Adeyanju walitoa taarifa kuhusu majadiliano kati yao na EFCC ambapo walielezea kwamba tume hiyo haikuwaelezea makosa halisi ya mteja wao.
Walitaka tume hiyo imwachilie bila masharti yoyote au itoe ushahidi utakaothibitisha haja ya kuendelea kumzuilia hasa baada ya kumhoji kwa saa kadhaa jana Mei 5, 2025.
Otse alikuwa ameandamana na mamake mzazi hadi kwenye benki ya GTB Ijumaa kuwasilisha malalamishi baada ya kudai kwamba pesa zilikuwa zikitolewa kwenye akaunti ya mamake bila maelezo faafu.
Sasa EFCC imesema kwamba VDM ataondoka kwenye afisi zao punde baada ya kutimiza masharti ya dhamana.