EACC yawaonya wawakilishi wadi dhidi ya kulazimisha kandarasi

Martin Mwanje
1 Min Read

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imewaonya vikali wawakilishi wadi na baadhi ya wafanyakazi wa mabunge ya kaunti dhidi ya kulazimisha utoaji wa kandarasi kinyume cha sheria.

Mkurugenzi wa EACC kanda ya magharibi, Erick Ngumbi, amesema kuwa baadhi ya wawakilishi wadi wamekuwa wakiwatishia magavana na maafisa wa kaunti kwa lengo la kulazimisha kupewa kandarasi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na maadili ya utumishi wa umma.

Tume hiyo imebaini kuwa vitisho hivi vinalenga kuwalazimisha magavana au maafisa wa serikali ya kaunti kutoa kandarasi kwa wawakilishi wadi au watu wanaohusiana nao.

Ngumbi pia alifichua kuwa EACC inawachunguza wawakilishi sita wa wadi kwa madai ya kuhusika na utoaji wa kandarasi za thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.4 kupitia kampuni 38, bila kuzingatia sheria na taratibu za ununuzi wa umma.

Aidha, aliongeza kuwa uchunguzi huo ni sehemu ya juhudi za EACC kuhakikisha uwajibikaji na kuzuia ufisadi katika ngazi ya serikali za kaunti.

Share This Article