EACC yawakamata maafisa 5 wa polisi kwa kuitisha hongo

Martin Mwanje
1 Min Read
Maafisa wa polisi waliokamatwa kwa madai ya kuitisha hongo

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) leo Alhamisi imewakamata maafisa watano wa polisi wa trafiki kwa kwa madai ya kuitisha hongo.

Waliokamatwa ni pamoja na Corporal Hezron Aburi, Corporal Mary Nabei, Police Constable James Weru, Police Constable Mwakwekwe Nyoka, na Police Constable Aisha Abdullahi.

Maafisa hao wanaofanya kazi katika kituo cha polisi cha Busia wameripotiwa kupatikana na kosa hilo kwenye kizuizi cha polisi kilichopo kwenye barabara kuu ya Kisumu–Busia, takriban kilomita tano kutoka mjini Busia.

Kukamatwa kwao kunafuatia madai yaliyokithiri kutoka kwa wahudumu wa magari na raia kwamba maafisa wanaosimamia vizuizi vya polisi kwenye barabara hiyo wamebobea katika kuitisha mlungula.

Wakati wa operesheni hiyo, maafisa hao walipatikana wakiitisha hongo kutoka kwa wahudumu wa magari waliongia au kuondoka mjini Busia, mara nyingi bila kufanya ukaguzi wowote au kutekeleza sheria za trafiki.

Washukiwa hao walipelekwa katika ofisi ya EACC ya kanda ya magharibi mjini Bungoma kuandikisha taarifa kabla ya kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Bungoma wakisubiri kufikishwa mahakamani.

Share This Article