Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imerejesha kipande cha ardhi ambacho thamani yake ni shilingi milioni 104.
Kipande hicho cha ekari 1.73 ambacho nambari yake ya usajili ni MN/VI/3748 kinapatikana mjini Mombasa.
Ardhi hiyo inamilikiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (KAA) na ilidaiwa kunyakuliwa na Agil Mahmud, ambaye awali alihudumu kama mratibu wa masuala ya ardhi katika uliokuwa mkoa wa pwani.

Kwenye uamuzi uliotolewa Julai 23, 2023, Jaji Kibunja wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi, Mombasa, alisema ardhi hiyo iliyotengewa shughuli a umma, haiwezi kutengewa watu binafsi.
Akifutilia mbali cheti cha hati ambacho kwa sasa kinashiliwa na kampuni ya Academy Properties Limited, mahakama ilisema kwa sababu utengaji wa awali wa ardhi hiyo kwa Agil Mahmud haukuwa halali na haukufuata utaratibu uliowekwa, uhamishaji uliofuata wa ardhi hiyo kwa watu wengiene hauna msingi.
Uchunguzi wa EACC ulifichua kuwa kipande cha ardhi ambacho nambari yake ya usajili ni MN/VI/3748 kilikuwa sehemu ya kipande cha ardhi ambacho nambari yake ya usajili ni MN/VI/3888, chenye ukubwa wa ekari 538.76.

Kulingana na uchunguzi huo, kipande hicho kilimilikiwa na Uwanja wa Ndege wa Port Reitz ambao kwa sasa unajulikana kama Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi uliopo chini ya (KAA).
Tume ya EACC bado inatafuta kurejeshwa kwa vipande vingine 12 vya ardhi, vyote vilivyotolewa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi vyenye thamani ya shilingi bilioni 2.5.