Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) imetajwa kuwa kizuizi kikubwa kwa juhudi zinazoendelea za kuangamiza jinamizi la ufisadi nchini.
Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inaituhumu ofisi hiyo, inayoongozwa na Renson Ingonga, kwa kile inachosema ni hulka ya kuondoa kesi za ufisadi zilizowasilishwa kwake na tume hiyo bila kutafuta ushauri wake.
Mwenyekiti wa EACC Dkt. David Oginde na Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo Abdi Mohamud wametoa mfano wa kesi za ufisadi 18 zilizowasilihwa kwa ODPP zikihusisha kaunti mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kaunti za Kericho, Embu, Isiolo, Makueni na Turkana miongoni mwa zingine.
Wakizungumza walipofika mbele ya Kamati ya Kaunti ya Uhasibu wa Umma ya Seneti leo Jumatano, wawili hao waliiambia kamati hiyo kuwa kesi dhidi ya kaunti hizo ziliondolewa bila kutafuta ushauri wa tume.
Kulingana nao, kesi dhidi ya washukiwa wa ufisadi huondolewa kufuatia maombi ya washukiwa hao.
Ni hali wanayosema huwalazimu kutumia njia za kiraia kurejesha mali ya umma iliyoibwa.
EACC sasa inatoa wito kwa bunge kuingilia kati ili kuhakikisha mwenendo wa ODPP unapigwa breki mara moja kabla ya vita dhidi ya ufisadi kwenda mrama.