EACC yachunguza madai ya rushwa katika taasisi ya KIHBT Kisii

Marion Bosire
2 Min Read
Fidel Omondi

Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC inachunguza madai ya utozaji na upokeaji rushwa katika taasisi ya mafunzo kuhusu teknolojia ya barabara kuu na ujenzi ya Kenya – KIHBT tawi la Kisii.

Maafisa wa EACC walitekeleza operesheni Novemba 28, 2025 baada ya tume kupata hati za upekuzi katika taasisi hiyo pamoja na makazi ya maafisa watatu wa KIHBT na mamlaka ya usafiri na usalama barabarani – NTSA.

Kwa mujibu wa EACC, uchunguzi huo ulifuatia ripoti kwamba wakufunzi katika Idara ya Uendeshaji Mitambo wamekuwa wakiomba rushwa kutoka kwa wanafunzi wanaopangiwa kufanya mitihani ya udereva inayosimamiwa na NTSA.

Inadaiwa wakufunzi hao hutoza ada ya kufanikisha ya shilingi 3,100 na wanaokataa kulipa hufelishwa mtihani moja kwa moja.

Wachunguzi wanasema mpango huo umekuwa ukiendeshwa na wakufunzi wawili, Philip Dawa na Fidel Omondi, ambao walikuwa wakigawana fedha hizo na wakaguzi wa NTSA.

Katika baadhi ya matukio, wanafunzi waliolipa rushwa walipata alama za kufaulu bila hata kufanya mitihani ya vitendo.

EACC pia ilifichua pia madai kwamba wakufunzi wamekuwa wakikusanya ada rasmi za shule kwa pesa taslimu na kupitia nambari zao binafsi za simu kinyume na kanuni zinazohitaji malipo kufanywa kupitia nambari rasmi ya taasisi.

Wanafunzi waliolipa karo moja kwa moja kwa wakufunzi husika walitozwa elfu 40, badala ya karo halisi ya elfu 65.

Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa Dawa ametekeleza miamala ya zaidi ya shilingi milioni 34 kupitia M-Pesa ndani ya miaka mitatu, huku Omondi akifanya miamala ya milioni 8 katika kipindi hicho.

Wakati wa operesheni, Omondi alikamatwa baada ya maafisa kupata shilingi elfu 171,000 ndani ya bahasha kwenye koti lake, pamoja na ushahidi mwingine muhimu.

Anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Kisii huku uchunguzi ukiendelea.

Share This Article