EACC yachunguza kesi za utakatishaji wa fedha

Marion Bosire
1 Min Read
Abdi Mohamud, Mkurugenzi Mkuu, EACC

Tume ya Maadili na Kupambana na uUisadi nchini, EACC, inaendelea kuchunguza kesi 32 za utakatishaji fedha.

Haya yalifichuliwa na Mkurugenzi Mkuu wa EACC Abdi Mohammud pembezoni mwa warsha ya kikanda jijini Nairobi kuhusu utakatishaji fedha na urejeshaji wa mali zilizoporwa.

Mohammud amesema tume hiyo imebaini watu binafsi wanaotakatisha fedha za umma na kuzihamishia nchi mbalimbali.

Kulingana na Chama cha Walipa Kodi nchini, NTA, Kenya hupoteza shilingi bilioni 253 kila mwaka kupitia mianya haramu ya kifedha.

Kampuni na watu binafsi wanaotakatisha mabilioni ya fedha za walipa kodi na kuzificha katika nchi zingine sasa wako chini ya uangalizi wa EACC.

Mohammud amesema tume hiyo kwa sasa iko katika mazungumzo na nchi kadhaa kupitia ushirikiano wa kisheria ili kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa, na hatimaye kuiondoa Kenya kwenye orodha ya nchi zenye hatari ya kifedha.

Warsha hiyo ya ngazi ya juu ya kikanda inalenga kuimarisha hatua za pamoja dhidi ya utakatishaji fedha na kuongeza ushirikiano katika ufuatiliaji, kushikilia, kunyang’anya na kurejesha mali zilizoporwa.

Nchi zinazoshiriki mkutano huo wa siku tatu ni pamoja na Uganda, Kenya, Zimbabwe, Madagascar, Namibia, Botswana, Rwanda, Tanzania, Ethiopia, Djibouti na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Share This Article