EACC yaangazia mafanikio yake katika ripoti ya mwaka

Marion Bosire
2 Min Read
Abdi Mohamud, Mkurugenzi Mkuu, EACC

Tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC, imeangazia mafanikio yake katika vita dhidi ya ufisadi kwenye ripoti yake ya mwaka wa kifedha 2024/2025.

Mafanikio hayo yalionekana hasa katika katika uchunguzi, urejeshaji wa mali, mageuzi ya kisheria na ushirikishaji wa umma ambapo jumla ya ripoti 4,183 za ufisadi zilipokelewa mwaka huo na uchunguzi ukaanzishwa kuhusu 1,846 kati yazo.

Utoaji na upokeaji rushwa ndio kosa lililoripotiwa zaidi kwa asilimia 37, ukifuatiwa na ubadhirifu wa fedha za umma kwa asilimia 19 na maadili yasiyo mema asilimia 13.

Kujipatia na kuuza mali ya umma kwa njia za udanganyifu ni asilimia 10 na uhalifu mwingine wa kiuchumi kama udanganyifu wa ununuzi, mgongano wa maslahi, matumizi mabaya ya mamlaka na utakatishaji fedha kwa asilimia 21.

EACC inaendeleza uchunguzi katika kesi 838 za ufisadi na uhalifu wa kiuchumi na iliwasilisha faili 175 kwa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma kwa hatua zaidi.

Kupitia oparesheni 14 na majaribio 166 ya uadilifu, tume hiyo ilizuia upotevu wa fedha za umma unaokadiriwa kufikia shilingi bilioni 16.5, kiwango cha juu zaidi katika miaka ya karibuni.

Kasi ya kufuatilia mali iliongezeka katika kipindi hicho ambapo EACC ilitambua mali 27 za thamani ya bilioni 22.9, ikazuia kupotea kwa mali ya thamani ya bilioni 2.685, ikafungua kesi 79 za kurejesha mali ya bilioni 4.8 na ikarejesha mali za umma zilizokuwa zimeibwa za thamani ya bilioni 3.4.

Katika matokeo ya kisheria, kesi 213 za ufisadi zilikuwa mahakamani. Kati yazo, 54 zilihitimishwa na kutoa hukumu 33 za hatia, 15 za kuachiliwa huru na 6 kuondolewa, hatua inayoashiria kuimarika kwa ubora wa kesi na ushirikiano na waendesha mashtaka.

Katika kulinda uadilifu kwenye utumishi wa umma, EACC ilitoa ushauri 134, ikafanya majaribio 166 ya uadilifu na kuchakata fomu 33,973 za kutangaza mali ya kibinafsi.

EACC pia ilifanya ukaguzi 2,783 wa uadilifu na kusababisha watu 50 kunyimwa nafasi za ajira kutokana na masuala ya uadilifu.

Share This Article