EACC, kaunti ya Baringo zazindua kamati ya kuzuia ufisadi

Martin Mwanje
1 Min Read
Kamishna wa EACC John Ogallo akiwa na Gavana Benjamin Cheboi wa Baringo

Kaunti ya Baringo imeelezea dhamira ya kuimarisha vita dhidi ya ufisadi kufuatia kuzinduliwa kwa Kamati ya Kuzuia Ufisadi ya Kaunti hiyo (CPC).

Uzinduzi huo uliofanyika katika makao makuu ya kaunti hiyo ni matokeo ya ushirikiano wa kimkakati kati ya Mamlaka ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na serikali ya kaunti ya Baringo.

Nao uliongozwa na kamishna wa EACC John Ogallo na Gavana Benjamin Cheboi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ogallo alilalamika kuwa ufisadi hudhoofisha demokrasia na kuchochea ukosefu wa usawa nchini.

Amesema kupitia kuzuia uovu huo, utamaduni wa uwazi unaweza ukakuzwa nchini kwa manufaa ya raia wote.

Gavana Cheboi aliunga mkono matamshi hayo akiahidi kuunga mkono kikamilifu utendaji kazi wa kamati hiyo.

Aliahidi kuwa utawala wake utatekeleza hatua za uzuiaji ili kuboresha uwazi na uwajibikaji katika utoaji huduma kwa raia.

Kulingana na Utafiti wa Maadili ya Taifa na Ufisadi wa mwaka 2024, kaunti ya Baringo inaorodheshwa ya pili katika utoaji rushwa kote nchini.

Share This Article