Duale, Magavana wavutana juu ya wahudumu wa afya wa UHC

Waziri wa Afya aliashiria Agosti 25 kuwa mapatano ya kuajiriwa kwa wahudumu wa UHC yameafikiwa kati ya serikali kuu na zile za kaunti, msimamo ambao Magavana wamekanusha.

Martin Mwanje
3 Min Read

Baraza la Magavana (CoG) limekanusha taarifa ya kuafikiwa kwa makubaliano kati yake na Wizara ya Afya juu ya kuajiriwa kwa wahudumu wa mpango wa utoaji afya kwa wote, UHC. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Afya ya baraza hilo Muthomi Njuki amesema ingawa wanakiri ushirikiano kati ya ngazi mbili za serikali katika kusimamia wahudumu wa UHC, Magavana hawakubaliani na taarifa iliyotolewa na Waziri wa Afya Aden Duale.

Kulingana na Njuki, taarifa ya Duale jana Jumatatu ilikinzana na msimamo ulioafikiwa kati ya serikali kuu na za kaunti.

“Kuhusu kuhamishwa kwa wahudumu wa afya wa UHC, ilikubaliwa kuwa Wizara ya Afya itatenga rasilimali za kutosha kwa mujibu wa kiwango cha mishahara kilichoidhinishwa na SRC kabla ya kuhamishwa kwa orodha ya malipo kwa serikali za kaunti. Kwa sababu mikataba yao bado ni halali, uamuzi wa kuhamisha wahudumu hao wakati huu unakuja mapema na kwa wakati usiofaa,” alieleza Njuki ambaye pia ni Gavana wa Embu.

“Kuhusiana na suala la kuthibitisha wahudumu wa afya wa UHC, ripoti kutoka kwa zoezi la uthibitishaji wa wahudumu wa UHC bado haijahalalishwa na kushirikishwa rasmi na kwa hivyo, mchakato wa uhamishaji ambao Wizara inapendekeza haujakubaliwa.”

CoG sasa inapendekeza kuwa serikali, kupitia Wizara ya Afya, itenge na kutoa rasilimali zinazohitajika kwa serikali za kaunti ili kuwezesha kuajiriwa kwa wahudumu wa UHC kulingana na sera ya idara ya wafanyakazi, HR ya kila kaunti.

“Ikiwa hilo halitatimia, kuajiriwa kwa wahudumu wa afya wa UHC hakutawezekana,” alitahadharisha Njuki.

Matamshi yake yanakuja siku moja baada ya Wizara ya afya kutangaza kuajiriwa kwa wahudumu wa afya chini ya mpango wa UHC baada ya ukaguzi uliotekelezwa kote nchini.

Kwenye taarifa, Duale alisisitiza kujitolea kwa serikali kuimarisha nguvukazi katika sekta ya afya ambayo ni nguzo kuu katika kuafikia mpango wa huduma za afya kwa wote na utoaji huduma bora kote nchini.

Alidokeza kuwa mpango wa ukaguzi wa wahudumu hao wa afya uliotekelezwa kwa pamoja na Idara ya Huduma za Afya na Baraza la Magavana ulilenga wahudumu 7,629.

Hata hivyo, wahudumu 215 hawakujitokeza kukaguliwa na wakatajwa kuwa wafanyakazi hewa au wasiohitimu. Mishahara yao imesimamishwa huku uchunguzi ukiendelea.

Waliopatikana kuwa sawa wamegawanywa katika makundi mawili, la wanaoendelea kuhudumu na la wanaokabiliwa na kesi za kinidhamu.

Waziri Duale alielezea kwamba walio kwenye kundi la kwanza watajumuishwa kwenye mfumo wa afya kuanzia mwezi Septemba mwaka huu wa 2025.

Waliosalia watasubiri uchunguzi kuhusu kesi zao za nidhamu kabla ya kufahamu hatima yao kulingana na kanuni za Tume ya Utumishi wa Umma, PSC.

 

 

Share This Article