Duale aahidi kuhakikisha wahudumu wa Afya wanasajiliwa kwenye SHA

Duale alisisitiza kuwa wahudumu wa afya wanastahili kupata ulinzi, manufaa na mifumo ya msaada sawa na ile wanayotoa kwa wengine.

Marion Bosire
2 Min Read
Aden Duale, Waziri wa Afya

Waziri wa Afya Aden Duale amesema kuwa Wizara ya Afya imejitolea kikamilifu kuhakikisha kuwa wahudumu wa afya wanajumuishwa kikamilifu katika Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA).

Akizungumza hapo jana, Duale alisema kuwa serikali imejitolea kutekeleza Mkataba wa Makubaliano ya Pamoja (CBA) na Chama cha Madaktari, Wataalamu wa dawa na Madaktari wa Meno wa Kenya – KMPDU.

Duale alisisitiza kuwa wahudumu wa afya wanastahili kupata ulinzi, manufaa na mifumo ya msaada sawa na ile wanayotoa kwa wengine.

Wakati huo huo, Waziri huyo alitoa wito kwa wataalamu na wahudumu wa afya kushirikiana kikamilifu na serikali katika kuunda na kutekeleza sera endelevu, za ndani ambazo zinaakisi changamoto za kipekee za afya zinazoikumba nchi.

Kwa upande wake Katibu wa Huduma za Matibabu, Dkt. Ouma Oluga, alisema kuwa serikali inaendelea kushiriki kikamilifu katika mashauriano yanayoendelea na mazungumzo yaliyopangwa na wadau wote wa sekta ya afya, ili kuunda mazingira ya kazi yenye msaada zaidi, haki na heshima kwa wataalamu wa afya.

Kuhusu suala la madaktari wanagenzi, waziri Duale alisema serikali inashughulikia mgogoro huo unaohusu wanagenzi wengi kuliko nafasi zilizopo, kucheleweshwa kwa ajira zao na usimamizi duni unaosababishwa na ujio usiodhibitiwa wa taasisi nyingi za mafunzo ya udaktari.

Duale alisema wanashirikiana na baraza la madaktari na wataalamu wa meno KMPDC kuhakikisha utekelezaji wa viwango vya ubora, kupanua vituo vilivyoidhinishwa vya uanagenzi na kuwianisha uajiri na bajeti.

Alisema kufikia sasa madaktari wanagenzi wapatao 1,035, wataalamu wa meno wanagenzi 83 na wataalamu wa dawa wanagenzi 503 wameandaliwa kwa ajira ambayo itaanza Julai mwaka huu wa 2025.

Waziri Duale alikuwa akizungumza huko Mombasa ambapo aliongoza kongamano la 9 la kila mwaka la wanachama wa KMPDU.

Share This Article