DRC na Rwanda kutia saini Makubaliano ya Amani

Tom Mathinji
2 Min Read
DRC na Rwanda kutia saini makubaliano ya amani.

Katika kile kinachoonekana kama hatua ya kusitisha mzozo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Rwanda na DRC zinalenga kutia saini makubaliano ya amani ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Hatua hiyo ni sehemu ya msukumo wa kidiplomasia wa kukomesha ghasia baada ya waasi wanaoungwa mkono na Rwanda kuendeleza mapigano mashariki mwa DRC.

Makubaliano hayo yanatoa matumaini ya kupungua kwa mzozo wa miongo kadhaa, huku nchi zote mbili zikitarajia kuvutia uwekezaji mkubwa wa Marekani katika madini.

Hata hivyo, wito wa siku za hivi karibuni  kuhusu usitishaji mapigano haujafanikiwa kumaliza mapigano ambayo yamekuwa yakiendelea kwa muda sasa.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili wanatarajiwa kutia saini makubaliano hayo mbele ya Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio.

Washington iko kwenye mazungumzo ya kuwekeza mabilioni ya dola katika madini nchini Congo, ambayo ina akiba kubwa ya shaba, cobalt na lithiamu, inayotumika katika simu za rununu na magari.

Rwanda ilisema wiki hii pia ilikuwa ikizungumza na Marekani kuhusu uwezekano wa makubaliano ya madini.

Congo imeshuhudia kuongezeka kwa ghasia baada ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kufanya mashambulizi makubwa mwezi Januari na kuteka miji hiyo miwili mikubwa mashariki mwa nchi hiyo.

Umoja wa Mataifa na serikali za Magharibi zinasema Rwanda imetoa silaha kwa waasi wa M23.

Hata hivyo, Rwanda inakanusha kuunga mkono M23 na inasema jeshi lake limejilinda dhidi ya jeshi la Congo.

Qatar na Marekani zimeonyesha nia ya kupatanisha azimio hilo.

Share This Article